Jeremiah 36

Yehoyakimu Achoma Kitabu Cha Yeremia

1 aKatika mwaka wa nne wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia nabii Yeremia kutoka kwa Bwana, kusema: 2 b“Chukua kitabu uandike ndani yake maneno yote niliyonena nawe kuhusu Israeli, Yuda na mataifa mengine yote, tangu nilipoanza kunena nawe wakati wa utawala wa Yosia hadi sasa. 3 cLabda watu wa Yuda watakaposikia juu ya kila maafa ninayokusudia kuwapiga nayo, kila mmoja wao atageuka kutoka njia zake mbaya, kisha nitasamehe uovu wao na dhambi yao.”

4 dHivyo Yeremia akamwita Baruku mwana wa Neria, naye Yeremia alipokuwa akiyakariri maneno yote aliyoyasema Bwana, Baruku akayaandika katika kitabu. 5Kisha Yeremia akamwambia Baruku, “Nimezuiliwa, mimi siwezi kuingia katika Hekalu la Bwana. 6 eBasi wewe nenda katika nyumba ya Bwana siku ya kufunga, uwasomee watu maneno ya Bwana kutoka kitabu hiki yale uliyoyaandika kutoka kinywani mwangu. Wasomee watu wote wa Yuda waliofika kutoka miji yao. 7 fLabda wataomba na kusihi mbele za Bwana na kila mmoja akageuka kutoka njia zake mbaya, kwa sababu hasira na ghadhabu zilizotamkwa dhidi ya watu hawa na Bwana ni kubwa.”

8Baruku mwana wa Neria akafanya kila kitu nabii Yeremia alichomwambia kufanya. Alisoma maneno ya Bwana katika Hekalu la Bwana kutoka kile kitabu. 9 gKatika mwezi wa tisa, mnamo mwaka wa tano wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati wa kufunga mbele za Bwana, ilitangazwa kwa watu wote walioko Yerusalemu, na wale wote waliokuwa wamekuja kutoka miji ya Yuda. 10 hKutoka chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruku akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu la Bwana maneno ya Yeremia kutoka kwenye kile kitabu.

11Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Bwana kutoka kwenye kile kitabu, 12 ialishuka hadi kwenye chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote: yaani Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na maafisa wengine wote. 13Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruku akiwasomea watu kutoka kwenye kile kitabu, 14maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruku, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu, nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruku mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake. 15Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.”

Ndipo Baruku akawasomea kile kitabu.
16Walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruku, “Lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.” 17Kisha wakamuuliza Baruku, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”

18 jBaruku akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”

19 kNdipo wale maafisa wakamwambia Baruku, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu yeyote asijue mahali mlipo.”

20Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu. 21 lMfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu. Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka kwenye chumba cha Elishama mwandishi, na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme. 22 mUlikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto. 23 nHata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni, hadi kitabu chote kikateketea. 24 oMfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonyesha hofu yoyote, wala hawakuyararua mavazi yao. 25 pHata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu, yeye hakuwasikiliza. 26 qBadala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli, na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruku na nabii Yeremia. Lakini Bwana alikuwa amewaficha.

27Baada ya mfalme kuchoma kile kitabu kilichokuwa na yale maneno Baruku aliyokuwa ameyaandika kutoka kinywani mwa Yeremia, neno la Bwana lilimjia Yeremia likisema: 28“Chukua kitabu kingine na uandike juu yake maneno yote yaliyokuwa katika kile kitabu cha kwanza, ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda amekiteketeza kwa moto. 29 rMwambie pia Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ulikiteketeza kile kitabu ukasema, “Kwa nini uliandika kwenye kitabu kwamba kwa hakika mfalme wa Babeli angekuja na kuangamiza nchi hii, na kuwakatilia mbali watu na wanyama kutoka humo?” 30 sKwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana kuhusu Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Hatakuwa na mtu yeyote atakayekalia kiti cha enzi cha Daudi; maiti yake itatupwa nje kwenye joto wakati wa mchana na kupigwa na baridi wakati wa usiku. 31 tNitamwadhibu yeye, watoto wake na watumishi wake kwa ajili ya uovu wao. Nitaleta juu yao na wote waishio Yerusalemu na watu wa Yuda kila maafa niliyoyasema dhidi yao, kwa sababu hawajasikiliza.’ ”

32 uKisha Yeremia akachukua kitabu kingine na kumpa mwandishi Baruku mwana wa Neria, naye kama Yeremia alivyosema, Baruku akaandika juu yake maneno yote ya kile kitabu ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda alikuwa amekichoma moto, na maneno mengine mengi yaliyofanana na hayo yaliyoongezewa humo.
Copyright information for SwhKC